Kiongozi wa chama cha TIP TIP Kalembe Ndile amependekeza kuwekwa kwa sheria kuwa wanaowania nafasi za uongozi waonyeshe ripoti ya daktari kabla ya kuruhusiwa kugombea nafasi hizo.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari katika hoteli moja jijini Mombasa siku ya Jumatatu, Ndile alisema baadhi ya viongozi huenda wako na matatizo ya kiakili kufuatia matamshi ya uchochezi wanayotoa kila mara.
Vile vile, alimtaka mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko kuagiza Seneta wa Machakos Johnson Muthama afanyiwe ukaguzi wa akili kabla ya kufunguliwa mashtaka ya uchochezi.
“Viongozi wa miungano ya kisiasa wanapaswa kuacha wanachama wao wanaotuhumiwa kuchochea wananchi kuwajibikia matamshi yao, kuliko kuwatetea kila wanapotaka kufunguliwa mashtaka,” alisema Ndile.
Wakati huo huo, kiongozi huyo wa TIP TIP alitoa changamoto kwa muungano wa Cord kueleza wananchi ni pesa ngapi zimechangishwa kwenye akaunti waliofungua kuchangia walimu na lini zitapeanwa kwa walimu.