Mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Mombasa Mohamed Hatimi amesema kuwa itakuwa vigumu sana kwa ndoto ya Gavana wa Kilifi Amason Kingi kuunda chama kimoja cha watu wa pwani.

Share news tips with us here at Hivisasa

“Hayo yalikuwa maoni ya Kingi mwenyewe na tunayaheshimu. Kile ambacho tunajuwa ni kwamba eneo hili liko ndani ya ODM,” alisema Hatimi.

Siku ya Jumapili Kingi alitangaza kuwa wao kama viongozi waliochaguliwa kutoka pwani wako kwenye mazungumzo ya kuunda chama kimoja cha kisiasa.

Kingi ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Kilifi alikuwa mstari wa mbele katika kupigia debe chama cha ODM wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Kingi pia amekuwa mstari wa mbele kutaka mkoa wa pwani kujitenga na Kenya kwa kile ambacho anasema kuwa eneo la Pwani limesahaulika na serikali zilizotangulia.

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho pia amekuwa akitaka pwani kujitenga. Wiki jana Kingi hakuwepo wakati wa uapisho wa Raila Odinga kama rais wa wananchi jambo ambalo ambalo pia limekashifiwa na baadhi ya viongozi.

Mchanganuzi wa kisiasa Rocha Chimera alisema kuwa itakuwa vigumu sana kwa eneo la Pwani kuunda chama kimoja  ikizingatiwa kuwa gavana Joho ni mfuasi sugu wa ODM.

Chimera alisema kuwa Kingi ana nafasi nzuri ya kuendelea kuongoza iwapo atasalia ndani ya mrengo wa NASA.

“Sidhani kama kuunda chama kimoja cha kisiasa cha pwani wazo kitamfanya kingi kuwa maarufu. Huenda hata akapoteza zaidi lakini akisalia katika muungano maarufu kote nchini itakuwa nafasi nzuri kwake kuendelea kuongoza,” alisema Chimera.