Sheikh Juma Ngao amejiuzulu kama mkurugenzi wa mamlaka ya Nacada.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Ngao alitangaza kujiuzulu kwake kutoka kwa wadhfa huo siku ya Ijumaa, kufuatia alichokitaja kama kuhangaishwa katika vita dhidi ya ufisadi.

Akiwahutubia wanahabari jijini Mombasa, Ngao alisema alilazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na hatua ya baadhi ya maafisa wa bodi hiyo kujihusisha katika maswala ya ufisadi.

“Ni wazi shirika la Nacada linajihusisha na ufujaji wa fedha za umma sawia na kutoa zabuni bila ya kufuata sheria ipasavyo. Hii ndio maana wanajaribu kujificha kwa kutishia viongozi wanaotambua ukweli huo,” alisema Ngao.

Aidha, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahusika, licha ya Tume ya EACC kuwasilisha ripoti yake kuhusiana na ufisadi katika shirika hilo.

Hata hivyo, Bwana Ngao ameapa kushikilia msimamo wake wa kutofumbia macho ufisadi katika ngazi zozote za uongozi huku akiutaja kama adui mkubwa wa maendeleo.

“Siwezi jiruhusu kuwa katika shirika linalotekeleza ufisadi, ndio maana nimeamua kutangaza rasmi kujiuzulu na kujiweka mbali na dosari la maendeleo,” alisema Ngao.