Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafugaji wa ng’ombe katika eneo la Mariakani wanakadiria hasara baada ya mifugo zaidi ya 20 kupatikana wakiwa wamefariki katika hali ya kutatanisha.

Kwa mujibu wa wenyeji, ng’ombe hao walifariki baada ya kula mifuko ya plastiki huko malishoni, kutokana na ukame ambao umechangia kukauka kwa nyasi eneo hilo.

Inadaiwa kuwa kisa hicho kilitokea baada ya ng’ombe hao kutoka malishoni, huku baadhi ya wakaazi wakidai kuwa huenda ng’ombe hao walikula nyasi zilizokuwa na sumu.

Hata hivyo, daktari wa mifugo katika eneo hilo alisema kuwa ulaji wa mifuko ya plastiki hauwezi kuwaua ng'ombe zaidi ya kumi kwa wakati mmoja kabla ya wafugaji kugundua.

Joseph Njirain, daktari wa mifugo katika eneo hilo la Mariakani, aliwaonya wenyeji dhidi ya kuwala mizoga hiyo.

Alisema kuwa wameanza uchunguzi kubaini chanzo maalum cha maafa ya wanyama hao, huku akiongeza kuwa hali hiyo huenda ilisababishwa na mkurupuko wa maradhi ya mifugo.

Aidha, wafugaji hao wameitaka Wizara ya Kilimo kuingilia kati ili kuwanasua kutoka hali hiyo, ili kuzuia hatarii zaidi.