Mkulima mmjoa katika eneo la Elementaita, eneo bunge la Gilgil kaunti ya Nakuru ametamaushwa na kisa cha ng'ombe wake wakike kuwageukia mifugo wenzake na kuanza kuwala.
Mkulima huyo, Charles Mamboleo, amesikitikia kisa hicho akisema kuwa wiki mbili zilizopita sasa ng'ombe huyo mla nyama amewaangamiza kondoo wake wawili.
Kisa hicho ambacho amekitaja kama cha kwanza kushuhudia maishani mwake kimemtia wasiwasi kwani kwa boma lake kuna watoto wachanga ambao humlisha ng'ombe huyo.
Mamboleo anaogopa kuwa huenda akawageukia watoto hao na kuwala.
Amesema kuwa atalazimika kutafuta ushauri kutoka kwa madaktari wa mifugo kuhusu tabia hiyo ya ng'ombe na kusema kwamba mnyama huyo huenda amekumbwa na matatizo ya kiakili.
Kulingana na mke wa Mamboleo, afisa wa kilimo Nyanchani, alidokeza kuwa tabia kama hizo si za kawaida na huenda ng'ombe huyo anakumbwa na ukosefu wa madini flani muhimu mwilini ikizingatiwa ana uja uzito wa miezi saba sasa.
Mkulima huyo ameingiwa na wasiwasi kwamba huenda ng'ombe huyo akawala watoto wake baada ya kujifungua kwani tayari amewala kondoo kadhaa.
Daktari alisema kuwa utafiti zaidi unahitajika ili kuthibitisha madai hayo.