Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amekana madai yaliyotolewa na baadhi ya vijana kuwa amewatenga.
Ngunjiri amesema kuwa hawezi watenga vijana kwani ni wao waliompa kura nyingi zaidi mwaka 2013.
Akizungumza katika eneo la Maili Sita Jumatatu Ngunjiri alisema kuwa madai hayo yanaendeshwa na wapinzani wake wanaolenga kumharibia sifa.
Alisema kuwa ameanzisha miradi mingi sana inayowalenga vijana na kuwa anaendelea kushirikiana na vijana kuboresha maisha yao.
"Mimi nilipewa kura nyingi sana na vijana na hakuna vile nitawatenga vijana. Kuna kazi kubwa ambayo tumefanya hapa na vijana na tunaendelea nayo," alisema Ngunjiri.
"Kuna watu hapa wanazunguka wakisema hakuna kitu nimefanyia vijana na nataka waje waone ile kazi tumefanya," akasema Ngunjiri.
Aliwashauri vijana kujiepusha na tabia ya kutumiwa na wanasiasa kuzua vurugu katika mkutano.
"Ukilipwa mia mbili kwenda kupiga kelele kwa mkutano ujue ni wewe unajiumiza na haitakusaidia kitu," aliongeza.