Mbunge wa Bahati Onesmus Kimani Ngunjiri amelaumu OCPD wa Bahati Dancun Nkuthu kwa kuzembea katika vita dhidi ya pombe haramu ambayo imepelekea kifo cha mwanaume mmoja mwenye umri wa makamu usiku wa kuamkia Ijumaa hii ni baada ya kubugia pombe haramu aina ya chang'aa katika kijiji cha HodiHodi, Kabatini eneo bunge la Bahati.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge huyo wa Bahati alisema kuwa amekuwa akijaribu kila mara na hata kumwandikia Inspekta mkuu wa polisi akitaka afisa huyo wa polisi apewe uhamisho lakini juhudi zake zimeambulia patupu.

''Hatuwezi kimya wakati afisa anazembea katika vita dhidi ya pombe haramu humu nchini na hata kusababisha maafa baada ya wakaazi kubugia pombe hii','alisema Ngunjiri aliyejawa na Ghadhabu.

Aliongeza kuwa katika eneo la Maili saba chifu wa eneo hilo pia anafaa kuachishwa kazi  kwani amezembea katika kumaliza pombe haramu eneo hilo.

''Mtu mwingine ambaye anafaa kuenda nyumbani ni chifu wa maili saba kwa sababu amefeli katika kukomesha pombe haramu eneo lake hata baada ya Rais kutoa amri kwamba pombe hiyo inafaa kukomeshwa,''alisema Ngunjiri.

Mbunge huyo wa Bahati ameapa kuwasilisha ombi kwa katibu katika wizara ya usalama wa ndani Karanja Kibicho ili hatua ichukuliwe dhidi ya maafisa hao wawili wa utawala.

Haya yalijiri hata baada ya wakaazi kufanya maandamano Ijumaa eneo hilo na kuingia hadi kituo kipya cha polisi cha Bahati  wakishinikiza kutiwa mbaroni kwa maafisa wote wa polisi wanaohudumu katika kituo hicho.

'Tunataka haki na hawa maafisa wote wa hapa Bahati wasimamishwe kazi manake ni wazembe katika vita dhidi ya pombe haramu ilhali inaendelea kuua watoto wetu''alisema mama mmoja mkaazi wa eneo hilo.

Hata hivyo mwakilishi wadi ya Kabatini Paul Thuo Mwangi aliingilia kati na kuwatuliza wakaazi hao.