Mbunge wa Bahati amepuuzilia mbali matamshi ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuhusu ziara za nje za rais pamoja na suala la mkopo wa Eurobond.
Akizungmza mjini Nakuru siku ya Jumanne, Kimani Ngunjiri alidai kwamba Odinga analenga kutimiza malengo fulani ya kisiasa akiangazia uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.
Ngunjiri alisema kwamba madai ya Odinga kuwa fedha za mkopo wa Eurobond zimefujwa ni uongo mtupu.
“Mambo ambayo Odinga amesema ni propaganda tupu na madai hayo hayana ukweli wowote. Propaganda hii ambayo ameleta ni kutokana na kuwa uchaguzi mkuu uko karibu na tunajua watu wanapenda uongo ambao unakaribia ukweli,” alisema Ngunjiri.
Alisisitiza kwamba mkaguzi mkuu wa hesabu alielezea bayana kuhusiana na utumizi wa fedha wa mkopo huo wa Eurobond.
Kwa sasa, amemtaka Odinga kujitokeza hadharani kutoa ushahidi kuhusiana na usemi wake kwamba fedha hizo zimefujwa.
“Mkaguzi wa hesabu ameweka bayana na kusema kuwa anajua jinsi fedha zote zilivyotumika. Odinga ambaye sasa ameitwa atoe ushahidi amekataa kukubali wito huo. Mimi nauliza, yeye anatoa wapi taarifa zake anazosema anazijua. Anafaa aweke taarifa yake hadharani,” alisema Kimani.
Haya yanajiri huku Waziri wa fedha Henry Rotich akisisitiza kwamba hakuna fedha zilizofujwa kutokana na mkopo huo wa Eurobond.
Muungano wa upinzani umekuwa ukisisitiza kwamba serikali haijawaeleza Wakenya jinsi mkopo huo ulivyotumiwa.