Idara ya mahakama sasa imetakiwa itekeleze hukumu ya kifo dhidi ya madereva wanaosababisha maafa huku wakiendesha magari wakiwa walevi.
Ni mwito ambao umetolewa na mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri katika mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru, huku akisema madereva hao wanafaa kufikishwa mahakamani kwa kosa la mauwaji na kisha kupewa adhabu ya kunyongwa.
‘Hawa watu wa matatu wanaowauwa watu kwa sababu ya kuwa walevi wanafaa kufikishwa mahakamani kwa kosa la mauwaji na kisha wanafaa kuhukumiwa wakati huo huo. Ukisha hukumiwa, wekwa kamba mara moja maneno hayo yakwishe,’ alisema Ngunjiri.
Alikariri kuwa maafa ya watu wasiokuwa na hatia wanaoacha familia zao yanasababishwa na utepetevu wa madereva hao na kutokana na jambo hilo, wanafaa kupewa adhabu hiyo kali.
Alisisisitza kwamba hakuna haja ya kuwapa watu hao vifungo vya gereza badala ya kuwapata na hatia hiyo na badala yake wanafaa kunyongwa.
‘ Hawa watu wanafaa washtakiwe. Kwa nini tutenge muda hapa nchini kwa watu kama hawa? Sidhani tuna nafasi ya watu kama hawa, wanahitaji mara moja kunyongwa. Wakishikwa na wakihukumiwe, hatutaki tena kwenda kuwalisha magerezani. Tunawalisha huko miaka arobaini tukiwapa chakula! Hiyo pesa tunawalisha ya nini? Kama ulifanya mambo haya, wewe uhukumiwe kunyongwa, wewe uondoke, nchi iendee. Hata nchi imejaa zaidi,’ alikariri Mbunge huyo.