Mbunge wa Bahati Onesmus Kimani Ngunjiri , mmoja wa wabunge waliouangusha mswada wa thuluthi mbili wa uwakilishi wiki jana siku ya Jumatano ameapa tena kuuangusha mswada huo utakapowasilishwa tena bungeni wiki hii siku ya Alhamisi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihojiwa na mwandishi huyu mjini Nakuru Jumatatu, Ngunjiri alidai kwamba iwapo mswaada huo utapasishwa, utaongezea idadi ya wabunge kuwa 450 hali anayosema ni mzigo mzito kwa mlipa ushuru hapa nchini.

‘"Akina mama watazidi kwa mia moja. Hil;o ndilo jambo nyeti ambalo linanifanya nisiunge mkono mswada huo. Matumizi ya kifedha yako juu, Tunatumia fedha nyingi ambazo zingeweza kurudi kwa Mwananchi. Mwananchi aweze kufanyiwa Maendeleo. Utaona ikifika Alhamisi hatawafika bungeni kupigia kura mswada huo," alisema Kimani.

Matamshi sawia yalitolewa na mbunge wa Njoro Joseph Kiuna ambaye pia alikuwa mmoja wa walioupinga mswada huo bungeni wiki jana.

"Ni kweli nilikuwa mmoja wa waliopinga mswada huo. Uchaguzi ni kwa hiari ta mtu. Kama ingekuwa kuteua au kuajiri watu, hilo lingekuwa swala lingine. Isitoshe, Wanawake ndio wengi hapa nchini na iwapo watataka kumchagua mwanamke, wanaweza kufanya hivyo," alisema Kiuna.