Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amewasuta wakenya walio na mazoea ya kusema serikali inapigwa wakati kiongozi au mwanasiasa anaikosoa, akisema huo si usaliti.

Kimani alisema, "Rais Uhuru amekuwa Magharibi mwa nchi juzi na kupeana miradi ya mamilioni ya pesa. Kuna tatizo lipi sisi kuuliza hapa kwetu ametuletea nini, kiasi cha mtu kuitwa msaliti?"

Alisisitiza kuwa rais Uhuru Kenyatta alichaguliwa kuhudumia wakenya wote wala sio jamii ya wakikuyu pekee.

Wakati uo huo aliitaka idara ya kukabiliana na ufisadi nchini EACC, kuwakamata na kuwashtaki maafisa wanaoitisha hongo kutoka kwa magari na wanabodaboda kwenye barabara ya Nakuru Subukia.

Akizungumza Ijumaa mkutanoni kwenye eneo lake la ubunge wadi ya Kabatini, Kimani alidhibitisha kupokea malalamishi chungu nzima kutoka kwa wahudumu wa boda boda na madereva wa magari ya abiria, kuhusu jinsi wanahangaishwa na maafisa fulani kutoka kituo cha polisi cha Bahati.

Wanabodaboda hao walitaja maafisa wawili kwenye kituo hicho, ambao huwakamata na kuzuilia pikipiki zao ‘bila makosa’ na kisha kuwaitisha shilingi elfu tano ili ziachiliwe.

Akiitaka EACC kuchunguza maafisa hao, Kimani alisema, "Namchangamoto inspekta jenerali mkuu wa polisi nchini Joseph Boinett kuwahamisha wawili hao mara moja."

Hata hivyo aliwataka wanaboda boda na madereva kuacha kutoa hongo kwa polisi, akisema pikipiki zao zikikamatwa atahakikisha zinaachiliwa bila ya kutoa chochote.

“Wakati mwingine nilipigiwa simu hapa mnahangaishwa na OCS. Sasa ameenda baada ya mimi kuingilia kati. Tafadhali nawaomba msitoe chochote; mwachie pikipiki na unipigie simu,” akasema mtunga sheria huyo aliyechaguliwa kwa chama cha TNA.