Mchanganuzi mmoja mashuhuri wa masuala ya siasa nchini amependekezea Wakenya mfumo anaosema ni suluhu kamili ya kumaliza kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili serikali ya makabila chache.
Huku akitaka mchakato wa kubadilisha katiba uanze mara moja, msomi na mchanganuzi wa siasa Profesa Mutahi Ngunyi amesema wakati Wakenya wangerudi katika serikali ya mseto ilioanzishwa rasmi hapa Kenya na aliyekuwa mpatanishi mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, umewadia tena na kwa mara ya mwisho kwani ni mfumo unaotumiwa na mataifa yaliyostawi katika nyanja zote na zilizo na usawa wa kutamaniwa na kupigiwa mfano kote ulimwenguni.
"Sababu moja Wakenya wanafaa kuendea mfumo wa serikali ya mseto ni kwamba ni suluhu kamili kwa suala la tangu jadi linalowagonganisha Wakenya vichwa kila mara na hilo ni tabia ya kabila mbili tu zenye pia zina idadi kubwa ya wapiga kura hali ambayo Wakenya sasa wanaijua kama 'tyranny of numbers'. Aje kwani? katika mfumo huo wa serikali ya mseto, inawezekana kwamba kila hatamu ya uongozi wa kila rais atakayekuwepo itapambwa angalau na kabila tano zinazoongoza katika serikali yake na wala si mbili tu kila uchaguzi mkuu," alisema Bw Ngunyi.
"Isitoshe, serikali ya mseto ni dawa ya utepetevu unaoletwa na siasa duni za serikali inayojazwa na wanasiasa wa chama kimoja na mwono mmoja wa masuala tata nchini. Kwa kifupi, serikali ya mseto Kenya ndiyo itakayoleta utendakazi ambao Wakenya wamekua wakililia tangu walipojinyakulia uhuru kutoka kwa mkoloni beberu, " aliongeza Bw Ngunyi.
Hata hivyo, mchanganuzi huyo alionya kuwa asichukuliwe na yeyote yule kama anayependekeza kiongozi wa Cord Raila Odinga arudi serikalini.
"Serikali ya mseto ninayopendekezea Wakenya wapendwa ni ya vijana tupu ikiwemo Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto na wengineo lakini si na Bw Raila Odinga kwani, kama ninavyosema kila mara, wakati wake wa kuwa serikalini umekwisha; ulikwisha zamani za kale," alisema Ngunyi.