Mbunge wa Nyaribari Masaba Elijah Moindi amejitetea dhidi ya utafiti wa Infotrack ambao ulimuorodhesha kuwa miongoni mwa wabunge ambao hawajafanya maendeleo yoyote katika eneo wanalowakilisha.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge Moindi ambaye aliongea katika mji wa Kisii na Waandishi wa Habari, aliwashtumu waliofanya utafiti huo huku akisema kuwa wangemshirikisha au wangeandamana waende katika eneo Bunge lake ili kuhoji wanaoishi eneo hilo.

Pia alisema kuwa watafiti hao wamekuwa wakitumiwa na wapinzani wake wa kisiasa ili kumharibia jina na kusema kuwa yeye kama Mbunge wa Nyaribari Masaba amefanya maendeleo mengi ikiwemo kujenga shule za upili na msingi na kushangaa ni kwa nini awakujumuisha miradi kama barabara, mabasi ya shule kwenye ripoti yao.

“Waliofanya utafiti huu wanatumiwa vibaya na wapinzani wangu wa kisiasa na wanataka kuniona nimeanguka. Nimejengea shule nyingi madarasa, nikanunua basi la shule ya Ichuni, nikalikarabati barabara ya Kiamokama na tayari mpango upo wa kuweka lami barabara hiyo,” aliongeza Moindi.

Bwana Moindi pia ametangaza nia yake ya kupigania kiti cha eneo Bunge hilo la Nyaribari Masaba katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017.

Mbunge huyo alikuwa anazuru eneo hilo kukagua miradi ambayo inaendelea katika eneo Bunge lake ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kiamokama kuelekea Ekorongo ambao unatarajiwa kuanza mwezi Juni.