Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro amesema kuwa hababaishwi na hatua ya baadhi ya wabunge kumtimua kama kiongozi wa Jumuiya ya Wabunge wa Pwani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mung’aro alisema kuwa anazidi kuwa maarufu licha ya kupigwa vita na wapinzani wake.

Akizungumza mjini Kilifi siku ya Jumatano, Mung’aro alisema kuwa atazidi kuunga mkono muungano wa Jubilee kwani muungano huo ndio wenye uwezo na nia ya kuwasadia wakaazi wa Pwani.

“Tumekuwa ndani ya upinzani kwa miaka mingi bila kufaidi lolote. Safari hii haturudi nyuma. Tuko ndani ya serikali na tutasalia ndani ya serikali hata baada ya uchaguzi,” alisema Mung’aro.

Aidha, mbunge huyo alisema kuwa hatambui Jumuiya ya Wabunge wa Pwani unaongozwa na Mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga, na kushikilia kuwa angali kiongozi na msemaji wa wakaazi wa Pwani.

Kauli ya Mung’aro inajiri siku chache tu baada ya kutofautiana na Mwinga kuhusu uwajibikaji katika hafla ya mazishi katika eneo bunge la Kaloleni.