Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nyamira Alice Chae ameomba gavana wa Kisii James Ongwae na mwenzake wa Nyamira John Nyagarama kumpa fursa kusuluhisha mzozo ulioko mpakani Keroka kati ya kaunti ya kisii na kaunti ya Nyamira.
Kulingana naye, magavana wa kaunti hizo mbili wameshindwa kuelewana kuleta amani katika mpaka huo, jambo ambalo limepelekea wengi kujeruhiwa.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika uwanja wa michezo wa Gusii, Chae alisema kuwa yeye akipewa fursa ya kumaliza mzozo huo atafanya mara moja, na hakutakuwa na mzozo wa aina hiyo tena.
“Nashangaa sana wakati magavana wawili; wa Kisii na Nyamira wanashindwa kutatua mzozo mpakani keroka na kupelekea wakazi kujeruhiwa kila wakati, mimi kama kiongozi naomba nipewe fursa nilete amani na maelewano bila ubaguzi wowote,” alisema Chae.
Aidha, Chae aliomba magavana hao kujaribu kila wawezalo kuhakikisha mji wa keroka umeinuka kimaendeleo, haswa kuweka miradi ya maji na ukarabati wa soko ili wafanyibiashara kufanya shughuli zao za kibiashara kwa mazingira mema.