Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametangaza kwamba atakubali kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 iwapo makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, wataapishwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Raila, ambaye alipinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1997, 2007 na 2013,  alisema yuko tayari kukubali kushindwa iwapo muungano wa Jubilee utaunga mkono shinikizo la Cord la kutaka makamishna wapya kuteuliwa.

Bwana Raila alikuwa akizungumza siku ya Alhamisi, siku mbili baada ya kuungoza muungano huo wa upinzani katika maandamano ya kushinikiza makamishna wa IEBC kuondolewa madarakani.

"Hatuwezi kwenda kwa mechi na mwamuzi ambaye anakubaliwa na upande mmoja. Timu zingine pamoja na mashabiki wamepinga kuwepo kwa mwamuzi huyu. Hatuwezi kubali makamishna hao kuendelea kuhudumu kwa vile hata kanisa limepinga hatua hiyo," alisema Raila.

Raila alisema kuwa watahakikisha kuwa makamishna wa sasa wa Tume ya IEBC walioko chini ya uongozi wa Isaack Hassan, wametumwa nyumbani.

"IEBC lazima ibanduliwe na makamishna wapya kuteuliwa. Hatua hiyo ikichuliwa, basi nitakubali iwapo nitashindwa katika uchaguzi nkuu wa mwaka 2017," alisema Raila.

Kiongozi huyo ana furahia uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa kutoka eneo la Kibera, ambapo alihudumu kama mbunge kwa miaka mingi.