Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa hana sababu ya kukwamilia madarakani iwapo atashindwa na upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kauli ya Kenyatta inajiri huku upande wa upinzani chini ya uongozi wa Raila Odinga, ukishinikiza kubanduliwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, kwa madai ya ubaguzi.

Akiwahutubia wakaazi wa Kisii, Uhuru alisema kuwa hatasita kustaafu na kuenda Kiambu iwapo Tume ya IEBC itatangaza mshindi tofauti.

"Mimi siogopi kupoteza katika uchaguzi. Ni wananchi ndio hufanya maamuzi na kama hawatanipigia kura, sina sababu ya kukwamilia madarakani. Uamuzi wa wananchi huwa muhimu katika taifa lolote lile,” alisema Uhuru.

Aliongoeza, "Mimi niko tayari kurudi Gatundu iwapo nitapoteza uchaguzi mkuu wa mwaka 2017. Hili silo suala la kufa na kupona. Maisha lazima yaendelee baada ya uchaguzi.”

Alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa kujibidiisha kutafuta kura badala ya kuilaumu Tume ya IEBC ambayo alisema haiko chini ya ushawishi wowote wa nje.

"Sina sababu yoyote ya kuingilia utendakazi wa bodi huru. Naheshimu sheria na haki zao lazima ziheshimiwe," alisema Uhuru.

"Sote tujibidiishe kutafuta kura badala ya kulenga tume lisilo na hatia. Atakayeshinda basi ataingia madarakani. Hakuna haja ya kupigana kwa sababu ya uchaguzi," aliongeza Uhuru.