Mwenyekiti wa bodi ya huduma za usambazaji maji ya lake victoria kusini LVWSB professa John Arap Koech amesema kwamba bodi yake ina mipango ya kusuluhisha mzozo baina ya serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii kuhusiana na mzozo unaohusu bodi ya maji.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Hii inajiri baada ya hatua ya serikali ya kaunti ya Kisii kuwaachisha kazi wakurugenzi wa bodi ya utoaji huduma za maji Gusii GWASCO bila kuishauri serikali ya kaunti ya Nyamira. 

Akiwahutubia wanahabari nje ya ofisi ya gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama siku ya Jumatano baada yake kufanya mkutano na gavana huyo ili kutafuta mbinu ya kusuluhisha mzozo huo, Koech alisema kwamba bodi yake ina mipango ya kusulihisha tofauti baina ya serikali hizo mbili. 

"Nimefanya kikao na Gavana Nyagarama na tayari amenihakikishia kujitolea kwake kuhakikisha kwamba tofauti za usimamizi wa bodi ya GWASCO baina ya serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii zinasuluhishwa na nitahakikisha hilo linatimia kwa maana bodi ya GWASCO inawapa huduma za maji wakazi wa kaunti hizo mbili," alisema Koech.

Koech aidha aliongeza kuwa tayari halmashauri yake imepata mfadhili wa kigeni atakayejenga bwawa kubwa la maji kule Bonyunyu kwenye eneo bunge la Mugirango magharibi, bwawa litakalogharimu shillingi Billioni 6. 

"Ni furaha yangu kutangaza wazi kwamba kama halmashauri ya utoaji huduma za maji mkoani Nyanza tayari tumepata mfadhili wa kigeni atakayejenga bwawa kubwa la maji kule Bonyunyu kwa kima cha shillingi billioni sita, na nina hakika bwawa hilo litasaidia pakubwa wakazi wa Gusii nzima," aliongezea Koech.

Ikumbukwe kuwa mkutano huo unajiri baada ya serikali ya kaunti ya Kisii kuwasimamisha kazi wanachama wa bodi ya utoaji huduma za maji Gusii GWASCO bila ya kuishauri serikali ya kaunti ya Nyamira ikizingatiwa kwamba kampuni ya GWASCO inamilikiwa na kaunti zote mbili.