Simon Sang ameunyakua tena wadhfa wa katibu wa chama cha Makuli nchini ‘Dock workers Union’ baada ya kukusanya jumla ya kura elfu 2,701 na kumlaza mpinzani wake Bakari Bweta aliyepata jumla ya kura 365 pekee.
Akiwahutubia wafanyikazi wa bandari katika makao makuu ya bandari hiyo mjini Mombasa siku ya Jumatano, baada ya kutangazwa mshindi katika wadhfa wa katibu mkuu uligombewa na watu wanne, Sang amesema kwamba lengo kuu la muungano huo mpya kwa sasa ni kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ili kusawazisha maswala muhimu yanayohusiana na usimamizi wa bandari ya Mombasa.
Sang amesema kwamba ni lazima rais Uhuru Kenyatta ahakikishe kwamba usimamizi wa bandari hiyo ya Mombasa unazingatia maslahi ya wafanyikazi na kuhakikisha kwamba maswala ya kazi yanajadiliwa kati ya pande zote mbili katika njia ya uwazi.
Aidha Sang amesema kwamba katika kipindi cha miaka mitano atakayoongoza kama katibu mkuu wa chama hicho cha makuli atashinikiza kupewa kazi za kudumu kwa wafanyikazi wanaohudumu kwa kandarasi na pia akaapa kushirikiana na serikali ili kuzuia migomo ya wafanyikazi bandarini humo.
Nitahakikisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano wafanyikazi wa bandari wamepewa kazi za kudumu ili wawezekujikimu kimaisha na familia zao na chama chetu tutahakikisha kuwa tumekitetea kikamilifu," alisema Sang.
Katika uchaguzi huo wa hapo jana Mohammed Sheria amechaguliwa kama mwenyekiti wa chama hicho baada ya kukusanya jumla ya kura 987.