Mbunge wa Borabu katika Kaunti ya Nyamira Ben Momanyi ameahidi kuwasaidia wanafunzi ambao hawakunufaika kupata pesa za ustawi wa maeneo bunge almaarufu CDF katika ugawi wa mwaka jana.
Mbunge Momanyi alisema kuwa wale walio na ulemavu na wanaotoka katika familia maskini watapata usaidizi ili kuendelea na masomo.
Akiongea mnamo siku ya Ijumaa katika mji wa Nyamira, Momanyi aliwapa walimu changamoto ya kutia bidii masomoni ili kuinua viwango vya elimu katika eneo bunge hilo.
“Kwenye matokeo ya KSCE ya mwaka 2014, miongoni mwa shule kumi bora katika Kaunti ya Nyamira, tano zilitoka katika eneo bunge la Borabu. Kwa hiyo nawaomba walimu watie bidii zaidi ili tuweze kufanya hata vizuri zaidi katika mtihani wa mwaka huu,” alisihi Momanyi.
Aliongeza, “Wanafunzi ambao hawakupata basari mwaka jana ndio watakuwa wa kwanza kunufaika katika mgao wa mwaka huu. Pia wale ambao ni walemavu na wanaotoka familia maskini watapata usaidizi wa pesa ili kuendelea na masomo.”
Momanyi aliwaomba washikadau wengine katika sekta ya elimu kwenye eneo hilo kuungana ili kuinua viwango vya elimu Borabu.
“Nawaomba wazazi, wasimamizi wa elimu katika eneo bunge hili na viongozi kufanya kazi pamoja na kutafuta njia mwafaka ya kuimarisha matokeo ya mtihani wa kitaifa katika eneo Bunge la Borabu,” alisema Momanyi.
Kwa upande mwingine, Mbunge huyo aliahidi kutengeneza barabara za eneo bunge lake ili kurahisisha uchukuzi wa watu na bidhaa ndani na nje ya eneo hilo la Borabu.