Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa ardhi kaunti ya Mombasa Anthony Njaramba amemkosoa mwanasiasa Suleiman Shahbal kutokana na kile alichotaja kama kujitafutia umaarufu wa kisiasa kwa kuwapotosha wananchi.

Njaramba alitoa kauli hiyo kutokana na hatua ya mwanasiasa huyo kujitokeza na kuongoza wakaazi wa mtaa wa Khadija katika maandamano ya kupinga mpango wa serikali ya kaunti wa kujenga nyumba za kisasa.

Akiongea mjini humo siku ya Jumatatu, Njaramba alisema Shahbal anawapotosha wananchi kwani mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi.

“Mimi siwezi kushinda nikiongelea mtu anayejitafutia umaarufu kupitia njia ambazo hazieleweki, hawa ni watu wanataka kutengeza majina wala hakuna msaada wanaoleta kwa watu," alisema Njaramba.

Njaramba aliongeza kuwa serikali ya kaunti imeanzisha mpango huo unaolenga kubadilisha makaazi ya watu lakini wanasiasa wanawadanganya wananchi wasiokuwa na ufahamu.

Wakati uo huo waziri Njaramba alitoa wito kwa wananchi kutembelea afisi za kaunti iwapo wana lalama zozote kuhusu mpango huo badala ya kuwafuata wanasiasa.

Mapema wiki hii serikali ya kaunti ilizindua mpango wa kujenga nyumba za kisasa ili kubadilisha taswira ya mji huo.

Wakaazi wanaoishi katika nyumba za sasa watahamishwa kwa muda ili kupisha ujenzi huo.

Mwanasiasa Suleiman Shahbal siku ya Jumatano aliongoza wakaazi wa mtaa wa Khadija katika maandamano akisema kuwa serikali ya kaunti ya Mombasa ina nia ya kuwadhulumu wananchi kwa madai kwamba inataka kuwasaidia.