Mbunge wa Nakuru mjini mashariki David Gikaria amemtaka mwakilishi wa wadi ya biashara Stephen Kuria kuungana naye katika juhudi zake za kuleta maendeleo katika eneo bunge hilo.
Gikaria alimsihi Kuria kukoma tabia ya kupinga juhudi zake za kukuza eneo bunge hilo.
Akiongea katika mtaa wa Free Area, Ijumaa mchana alipozindua ujenzi wa choo cha umma, Gikaria alisema kuwa vita vya maneno kati yake na Kuria havitasaidia wakazi wa eneo hilo.
“Mimi kama mbunge wenu nataka kusema kuwa sina shida yeyote na MCA Kuria, niko tayari kushirikiana naye katika kuleta maendeleo Nakuru mashariki na ndiposa natoa wito kwa bwana Kuria aje tufanye kazi pamoja,” alisema Gikaria.
Gikaria alisema kuwa hana kinyongo na mtu yeyote na hawezi kumzuia mtu kuwania kiti cha ubunge cha Nakuru mashariki iwapo anataka.
“Mimi sina uwezo wa kumkataza mtu kuwania ubunge kama ana haja maanake watu watakao toa uamuzi ni wapiga kura bali sio Gikaria,” alisema
Gikaria na Kuria wamekuwa wakivuta pande tofauti kuhusiana na maswala muhimu ya kaunti ya hivi punde ikiwa ni shuguli ya kuwahamisha wachuuzi kuhama katikati mwa mji wa Nakuru.
Gikaria alikuwa katika mstari wa kwanza kupinga shughuli hiyo ilhali Kuria aliiunga mkono.