Muungano wa Cord umemuonya Waziri wa usalama Joseph Nkaissery dhidi ya kuendesha taifa kama kambi ya jeshi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Muungano huo umemtaka waziri huyo kufuata kanuni za katiba.

Kinara wa Cord Raila Odinga alimtaka Nkaissery kutowatishia viongozi wa muungano huo hasa wanapotekeleza majukumu yao ya kutetea wananchi wa taifa hili.

Akizungumza katika eneo bunge la Malindi siku ya Ijumaa, wakati wa mkutano wa maombi ya amani, Raila alidai kuwa kukamatwa kwa wabunge na maseneta wa Cord ilikuwa njama ya kuwanyamazisha.

“Ipo haja ya idara ya polisi kufanyiwa marekebisho kwa kuwa kwa sasa idara hiyo bado iko na mienendo ya ukoloni,” alisema Raila.

Aidha, kinara huyo alishikilia msimamo wake wa kubanduliwa kwa makamishna wa IEBC.

Wakati huo huo, alimtaka mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya uwiano na maridhiano, NCIC Francis ole Kaparo kukoma kuwatishia wananchi.

Raila pia aliwahimiza Wakenya kukumbatia umoja na amani na kutokubali kugawanywa kwa misingi ya kikabila.