Waziri wa ulinzi Joseph Nkaisserry na Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinnet huenda wakajipata pabaya, baada ya Jaji Isaac Lenaola kuamuru kuwa mbunge Timothy Bosire arejeshewe walinzi wake mara moja au watiwe mbaroni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Bosire ameomba mahakama iwasukume jela Nkaissery na Boinnet kifungo kisichozidi miezi sita kwa kukaidi agizo la kumrudishia walinzi wake. 

Bosire aliwasilisha ombi mahakamani kuwafungulia mashtaka wawili hao kwa kukuaidi amri ya koti kwa kutomrudishia mlinzi wake vile mahakama iliamuru. 

Kesi hiyo ilipowasilishwa mbele ya Jaji Mumbi Ngugi hapo awali hakutoa maagizo yoyote ila aliamuru kesi hiyo isikizwe na Jaji Isaac Lenaola, aliyeamuru walinzi wa Bosire warudishwe mara moja. 

Mbunge huyo anadai maagizo ya mahakama yalikiukwa kwa ukatili mkuu, huku akiongeza kuwa iwapo mahakama haitachukua hatua bado maafisa hao wakuu wa Serikali wataendelea kuisusia agizo hilo.

Wakili wa Bosire alisema kwamba maagizo ya mahakama hayatolewi tu kwa mzahaa bali yafaa kufwatwa na kutiliwa maanani. 

“Maagizo ya mahakama hayatolewi kwa ubatili. Lazima mahakama ihakikishe maagizo yake yametekelezwa kwa lengo la kudumisha hadhi yake,” alisema wakili Stephen Ligunya.