Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Joshua Nkanatha amesema kuwa vita dhidi ya pombe haramu vitaendelezwa hadi pale atakapohakikisha kuwa hakuna vifo vitakavyosababishwa na pombe hiyo.
Akizungumza kwenye maadhmisho ya siku ya Jumhuri siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Nkanatha alisema kuwa licha ya kampeni ya kukabiliana na pombe hatamu iliyoanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta hapo awali kutamatika, vita hivyo havitokoma kwenye kaunti ya Nakuru.
Aidha, alisisitiza kwamba doria za kukomesha ugemaji na uuzaji wa pombe haramu pamoja na zile za kiwango cha second generation zitazidishwa.
Nkanatha alisema kuwa kamati za kusimamia utoaji wa leseni, kudhibiti uuzaji, usambazaji na kutayarisha vileo katika kaunti ya Nakuru zilizozinduliwa rasmi na Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua siku ya Ijumaa wiki iliyopita, zitasaidia pakubwa katika kuhakikisha pombe hizi haramu zimemalizwa kabisa katika kaunti hii.
“Kuhusiana na maswala ya ulevi na ya vinywaji ambavyo vimepigwa marufuku tunazidi kusema tuko macho. Tuna kikosi maalum ambacho kiliundwa cha kusaidia kukabiliana na pombe haramu. Kamati hizo zitasaidia kuhakikisha kuwa hakuna vifo vinavyotokana na unywaji wa pombe haramu . Kampeni ambayo ilitangazwa na rais ya kukabiliana na pombe haramu ingali iko,” alisema Nkanatha.