Tume ya kitaifa ya ardhi nchini NLC, ikiongozwa na mwenyekiti Dr Mohammed Swazuri imeandaa vikao maalum kutatua mswala ya ardhi katika ukumbi wa taasisi ya Kenya School of Government, Mombasa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vikao hivyo vimewashirikisha moja kwa moja wakaazi wanaoishi katika ardhi zenye utata na ambazo zimekumbwa na migogoro katika maeneo tofauti ikiwemo Vikatwani, Kongowea na Karama.

"Kikatiba tume ya ardhi imepewa uwezo wa kupiga msasa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwakumba wakaazi katika sehemu tofauti za nchi, hasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuidhinisha marekebisho ya kipengee cha umiliki wa ardhi nchini,” alisema Swazuri.

"Yeyote anayekaa katika ardhi kiharamu anafaa kutolewa kisheria, lakini kwa sababu kuna maskwota humu nchini, tume hii imepewa wadhifa wa kuleta maelewano kwa kufanya mazunguzo na pande husika,” aliongeza.

Aidha, Swazuri alisisitiza kuwa tume hiyo itasaidia kutoa suluhu kwa migogoro ambayo imechukua muda mrefu kusuluhishwa katika mahakama, ikizingatiwa kuwa baadhi ya migogoro hiyo imekuwa katika mahakama tangu miaka ya kenda mia, bila suluhu kupatikana.

Tume hiyo imeratibu kuendelea na vikao hivyo hadi siku ya Alhamisi.