Mzozo kuhusiana na unyakuzi wa ardhi ya umma katika mtaa wa Naka, karibu na Section 58 unaendelea huku tume ya ardhi nchini NLC ikipendekeza mashamba hayo kurejeshewa umma.
Kupitia nakala ya mapendekezo yake kuhusiana na mzozo huo, NLC imeelezea wazi jinsi ardhi zilizotengewa ujenzi wa shule ya chekechea, ya msingi, ya upili, kanisa, ukumbi wa kijamii pamoja na uwanja wa kuchezea zimenyakuliwa na watu binafsi.
Mashamba hayo yalitengwa wakati wa ugavi wa shamba hilo mwaka wa 1987, lakini tume hiyo imefichua kuwa sasa stakabadhi zake zinaonyenyesha ni mali ya watu binafsi ambao wametakiwa kufafanua jinsi walijipatia mashamba hayo.
Mashamba hayo yalisimamiwa na iliyokuwa manispaa ya mji wa Nakuru ambayo sasa ni kaunti ya Nakuru, huku tume ya ardhi ikisisitiza kuwa mali ya umma sio ya watu binafsi.
"Hati zote za umiliki wa ardhi hizo za umma zitwaaliwe na kurejeshewa serikali ya kitaifa ambayo inasimamia shule za umma na zingine zirejeshewe serikali ya jimbo la Nakuru," ilisema NLC.
Mzozo wa ardhi katika mtaa huo haswa unyakuzi wa uwanja wa shule ya msingi ya Naka umekuwepo kwa muda mrefu sasa na haujapata suluhu kamili.
Juhudi za mwandishi huyu kuongea na afisi ya Gavana wa Nakuru au waziri wa ardhi kwenye jimbo ili kutoa ufafanuzi kamili hazikuzaa matunda.