Mzozo kuhusu usimamizi wa chama cha TNA tawi la Nakuru kati ya viongozi wawili, sasa umefika kikomo.
Aliyekuwa kaimu mwenyekiti wa chama hicho kwa muda Dkt Abdul Noor aliamua kung’atuka mamlakani kwa hiari yake.
Noor alisema hatua inapania kuzuia mizozo ya mara kwa mara.
Akiongea katika afisi za TNA mjini Nakuru siku ya Ijumaa, Noor alisema mvutano kuhusu kiongozi rasmi wa chama hicho huenda ukasambaratisha hata wafuasi wa chama hicho.
“Tumekuwa tukibakia kwenye mzozo katika kaunti yetu ya Nakuru. Vyombo vya habari vimekuwa vikisema TNA ina vita katika kaunti hii, na kwa sababu ya kupenda wananchi wa kaunti ya Nakuru na pia kumpenda rais wa nchi hii, siwezi kukubali ofisi yake ionekane kwamba ndio inayosheheni migogoro,” alisema Noor.
Hata hivyo, alidokeza kwamba yuko tayari kujiunga na muungano wa JAP, mwelekeo utakapotolewa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto ambaye ni kinara wa chama cha URP.
“Kuitwa mwenyekiti hauna maana kuliko kuhudumia wananchi wa kaunti ya Nakuru haswa wafuasi wa TNA. Kwa hivyo, mimi mwenyewe ndiye nimeamua kujiondoa kwa hiari niache mambo ya TNA yaendelee vizuri, lakini sijahama kwa chama,” alisema Noor.
Kwa miezi kadhaa chama hicho kimekuwa na mzozo kuhusu ni nani kiongozi rasmi kati ya Abdul Noor na Harrison Muiruri huku kila mmoja akishikilia ndiye mwenyekiti halisi.