Aliyekuwa mwenyekiti wa TNA Nakuru Abdul Noor ametoa wito kwa mshirikishi wa usalama kanda ya bonde la Ufa Wanyama Musiambu kuheshimu maoni ya kila mkaazi wa kaunti ya Nakuru kuhusiana na maswala ya usalama.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika mahojiano na vyombo vya habari Nakuru Jumatatu,Noor alisema kuwa kuna umuhimu wa Musiambu kusikiza maoni ya kila mkaazi kwa mujibu wa katiba kwani maoni kama hayo yanaweza kuwa na umuhimu katika maswala ya usalama na amani kanda hii.

''Ningependa kumhimiza mshirikishi wa kanda hii Wanyama Musiambu kuhakikisha kwamba anaskiza maoni ya kila mtu humu nchini pasina kujali kabila au dini,"alisema Noor.

Wakati huo huo, Noor alimpongeza Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kwa kuandaa hafla ya maombi ya shukrani katika kaunti ya Nakuru na kuhimiza amani na maridhiano.

Kwa mujibu wake kaunti ya Nakuru pia iliathirika na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008 na ujumbe wa maridhiano na msamaha ni muhimu kwa kila mmoja katika kuunganisha jamii.

Aliongeza kuwa ana imani na usemi wa Rais kwamba IDPs wote watafidiwa na serikali.

"Naunga mkono usemi wa Rais kuhusiana na maswala ya wakimbizi na najua atatekeleza kama alivyosema na ningependa kuwaomba wakaazi wote wa Nakuru kwamba tuunge mkono serikali katika juhudia za maridhiano na msamaha kwa mustakbali wa Kaunti ya Nakuru na taifa kwa jumla,''alisema Noor.