Tume ya Huduma kwa Polisi nchini NPSC imewaonya wahudumu wa magari ya umma hasa madereva na utingo wao dhidi ya kutoa hongo kwa maafisa wa trafiki.
Mwenyekiti wa tume hiyo nchini Johnston Kavuludi, amesema kuwa wamebaini kuwa maafisa wa trafiki huwatumia vibaya wahudumu wa matatu, huku wengine wakiwatishia kuwafikisha mahakamani iwapo watakaidi kutoa rushwa.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumanne wakati wa zoezi la kuwapiga msasa maafisa hao wa trafiki, Kavuludi alisema kuwa kamwe ufisadi hautaisha iwapo wakaazi wenyewe watashiriki ufisadi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa tume hiyo haitakubali hali hiyo kuendelea kushudiwa nchini.
Aidha, alidokeza kuwa maafisa wa tume hiyo wako nyanjani na atakayepatikana atachukuliwa hatua za kisheria.
"Tayari maafisa wetu wapo nyanjani kuendeleza uchunguzi wao na atakayepatikana lazima hatua kali za kisheria zitachukulia dhidi yake",alisema Kavuludi.
Zoezi hilo la kuwapiga msasa maafisa wa polisi wa trafiki limeingia wiki yake ya pili sasa huku maafisa 140 wakiwa tayari wamepitia vikao hivyo.