Wanasiasa wameombwa kueneza jumbe za amani na utangamano nchini, ili kudhibiti visa vya chuki za kikabila vinavyo weza ibuka wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika hafla ya mchango katika eneo la Manga siku ya Jumamosi, mwenyekiti wa Tume ya kuidhinisha katiba nchini CIC Charles Nyachae, alisema kuwa viongozi wanaosambaza jumbe za chuki za kikabila miongoni mwa wananchi wanafaaa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
"Wanasiasa wanao eneza jumbe za chuki za kikabila miongoni mwa Wakenya wanafaa kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria ili wawe funzo kwa wengine," alisema Nyachae.
Nyachae vilevile aliwasihi viongozi wa miungano ya kisiasa ya Cord na Jubilee kudadisi matamshi ya wanachama wao kwenye mikutano ya hadhara kwa minajili ya taifa.
"Sisi sote ni Wakenya tunaoishi kwenye taifa moja. Siasa za kikabila na uchochezi hazifai kuwa miongoni mwetu. Sisi kama viongozi tunafaa kuongoza taifa hili kwa njia nzuri na ushauri wangu kwa Cord na Jubilee ni kuwa sharti wanasiasa wa miungano hiyo waache kueneza jumbe za chuki ili kuimarisha utangamano,” alisema Nyachae.
Aliyekuwa spika wa bunge la kitaifa Kenneth Marende aliipongeza tume ya maridhiano na utangamano nchini NCIC kwa juhudi za tume hiyo kukabiliana na wanasiasa wachochezi nchini.
"Naipongeza tume ya utangamano na maridhiano NCIC kwa juhudi zake zakupambana na wanasiasa wachochezi nchini, ila naipa changamoto afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kufanya kazi kwa kushirikiana na tume hiyo ili kuhakikisha kuwa wanasiasa wachochezi wanafunguliwa mashtaka,” alisema Marende.