Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameiagiza idara ya mawasiliano na teknolojia katika kaunti ya Nyamira kuhakikisha kuwa inachapisha ripoti kwenye mtandao wake kuhusiana na utendakazi wa kila wizara.
Akihutubu kwenye mkutano wa uliojumuisha mawaziri, makatibu na wakurugenzi wa idara mbalimbali kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumatano, Nyagarama alisema kuwa hatua hiyo itasadia wananchi kufahamu jinsi wizara mbalimbali katika serikali yake zinavyofanya kazi.
"Nimeiagiza idara ya mawasiliano na teknolojia ICT kuhakikisha kwamba ripoti ya utendakazi ya kila wizara kwenye serikali yangu zinachapishwa kwenye mtandao wa idara hiyo ili kuwawezesha wananchi kufahamu jinsi wizara mbalimbali zinavyotelekeza majukumu," alisema Nyagarama.
Nyagarama aliongeza kusema kuwa serikali yake ina mipango ya kulipa mishahara mara dufu kwa wafanyikazi wote wa wizara itakayokuwa imefanya vizuri kuliko zingine kama njia yakuwapa motisha.
"Tumeweka mipango ya kulipa mishahara mara dufu kwa wafanyikazi wa wizara yeyote ile itakayokuwa imetekeleza majukumu yake vizuri kuliko zingine," aliongezea Nyagarama.