Kwa mara nyingine gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kusema kuwa mzozo wa eneo la Keroka unasababishwa na serikali ya kaunti ya Kisii. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye mahojiano na mtangazaji wa kituo cha radio cha Egesa Lawrence Nyakundi mapema Alhamisi, Nyagarama alisema kuwa mzozo wa kimpaka katika eneo la Keroka unatokana na hatua ya kaunti ya Kisii kuingilia eneo la Gusii. 

"Mzozo wa kimpaka ambao tunaendelea kushuhudia kule Keroka unatokana na hatua ya serikali ya kaunti ya Kisii kuanza kuingilia sehemu inayomilikiwa na serikali ya kaunti ya Nyamira," alisema Nyagarama. 

Nyagarama aidha aliongeza kwa kusema kuwa sehemu ya ardhi inayomilikiwa na serikali ya kaunti ya Kisii katika eneo la Keroka ni ndogo mno na haelewi sababu ya watu wa kaunti hiyo wanaendelea kuwashambulia wafanyakazi wa Nyamira. 

"Kilicho wazi ni kwamba eneo linalomilikiwa na serikali ya kaunti ya Kisii kule Keroka ni ndogo sana, na ndio maana kwenye makubaliano ya pamoja tuliyo yafanya na kaunti ya Kisii tulikubaliana kwamba serikali ya kaunti ya Nyamira iwe ndiyo inayostahili kukusanya ushuru, na sasa sielewi sababu ya kaunti ya Kisii kuendelea kuzua vurugu," aliongezea Nyagarama. 

Akizingumzia suala la kumaliza mzozo wa kimpaka katika eneo hilo, Nyagarama alisema kuwa serikali yake tayari imemwandikia barua mkurugenzi wa usoroveya kule Nairobi ili kuitaka ofisi hiyo ichukue jukumu la kufanya usoroveya katika eneo hilo. 

"Naona kwamba mahali imefikia ni kwamba ili kusuluhisha mzozo wa kimpaka kati ya serikali yangu na ile ya Kisii sharti ofisi ya mkurugenzi wa usoroveya humu nchini ichukue hatua ya kupima ardhi kule Keroka na ndio sababu tayari tumemwandikia barua mkurugenzi wa idara hiyo kutaka msaada," alihoji Nyagarama.