Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameshtumu vikali hali ya kupotea kwa nguvu za umeme kwenye sehemu kadhaa katika kaunti hiyo.
Akihutubu mjini Nyamira siku ya Jumatano, Nyagarama alilalamikia hali ya kupotea kwa nguvu za umeme, huku akisema kuwa hali hiyo inawasababishia wenyeji hasara kubwa.
Nyagarama aidha aliisihi kampuni ya usambazaji wa nguvu za umeme nchini kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali hiyo.
"Watu wetu wanaendelea kuteseka kutokana na kupotea kwa nguvu za umeme katika vituo vingi vya kibiashara, hali inayowasababishia hasara kubwa na sharti kampuni ya usambazaji umeme ichukue hatua madhubuti kuhakikisha kuwa hali hiyo imerekebishwa," alihoji Nyagarama.
Nyagarama aidha alisema kuwa serikali yake ina mipango ya kuezeka mtambo wa nguvu za jua katika eneo la Sironga ili kuwawezesha wakazi wa kaunti hiyo kupokea umeme kwa urahisi.
"Serikali yangu na kampuni moja ya 'Solar Power' kutoka nchini Uchina ina mipango ya kuezeka mtambo wa nguvu za kutumia miale ya jua katika eneo la Sironga ili kuwawesha wenyeji wa kaunti hii kupata umeme kwa urahisi," aliongezea Nyagarama.