Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kusuta madai ya kuwatenga vijana kwenye nafasi za ajira.
Akihutubu kwenye shule ya upili ya Sironga siku ya Alhamisi wakati wa mkutano wa pamoja uliowahuzisha mawaziri pamoja na wananchi, Nyagarama alisema kuwa serikali yake imewapa vijana kipau mbele kwenye nafasi za kazi.
"Hii dhana kwamba serikali yangu inawatenga vijana kwenye nafasi za ajira ni za uongo kwa maana tayari serikali yangu kupitia bodi ya uajiri wa wafanyakazi PSB imeajiri walimu 406 wa shule za chekechea, na tuna mipango ya kuajiri wengine zaidi," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliwarai wananchi kujitokeza kuripoti visa vyovyote vya ufisadi vinavyowahusisha maafisa wa serikali.
"Ni ombi langu kwenu wananchi kuhakikisha kuwa mnashirikiana nami kuvikabili visa vya ufisadi, na mapendeleo kwenye nafasi za ajira kwa kuripoti maafisa wanaojihisha na mambo hayo kwa maana mkinyamaza siwezi fahamu," aliongezea Nyagarama.