Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameshtumu kitendo ambapo mfanyakazi wa kaunti ya Nyamira alishambuliwa na watoza kodi wa serikali ya kaunti ya Kisii waliomwacha muathiriwa na majeraha mabaya katika soko la Keroka mapema Jumanne. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira, Nyagarama alikitaja kitendo hicho kuwa cha ukatili, huku ikizingatiwa kwamba soko hilo liko katika himaya ya kaunti ya Nyamira. 

"Ni aibu kwamba watu tunaowashuku kuwa watoza kodi wa serikali ya kaunti ya Kisii wanaweza mpiga na kumuumiza vibaya mmoja wa wafanyakazi wetu eti kwa sababu ya kuchukua hatua ya kufagia sehemu ya soko la Keroka," alishangazwa Nyagarama. 

Nyagarama aidha aliongeza kwa kuwaonya wahusika waliosababisha vurugu katika soko hilo, huku akihoji kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

"Tayari uchunguzi umeanzishwa kubaini wahusika waliosababisha vurugu mapema leo kwenye soko la Keroka, na wale watakaopatikana kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria," alionya Nyagarama. 

Ikumbukwe kuwa kwa muda sasa serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii zimekuwa zikizozania mji huo wa Keroka, huku kila moja ikidai kwamba mji huo uko kwenye himaya yao.