Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema tume ya elimu ya vyuo vikuu nchini CUE ilikosea kutoa ilani ya kufunga mabewa kumi ya chuo kikuu cha Kisii bila ya kuwashauri washikadau husika. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubu kwenye hafla ya mazishi ya nduguye mbunge wa Borabu Ben Momanyi kule Nyainagu katika eneo bunge la Borabu siku ya Jumatatu, Gavana Nyagarama alihoji kuwa tume ya CUE ingewashauri viongozi wa Gusii kabla ya kuchukua hatua hiyo.

"Ni jambo la kushangaza kwamba tume ya CUE inaweza chukua hatua ya kutaka kufunga matawi kumi ya chuo kikuu cha Kisii bila hata ya kutushauri sisi viongozi wa eneo hili," alisema Nyagarama. 

Nyagarama aidha aliongeza kwa kuwasihi wanasiasa kuwaheshimu viongozi waliochaguliwa huku akiwasuta wale wanaomshtumu kwa kutotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, suala alilosema ni la uongo na lenye nia ya kumharibia jina.

"Kuna watu wanaoendelea kuwadhalilisha viongozi walioko mamlakani ila nawashauri kuwaheshimu viongozi hao kwa maana walipewa majukumu na wapiga kura na kwa wale wanaofikiria kuwa wataniharibia jina eti kwamba sijatekeleza miradi ya maendeleo nawapa changomoto ya kutaja miradi ya maendeleo ambayo wao wenyewe wametekeleza," alihoji Nyagarama.