Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewahakikishia wakazi wa kaunti hiyo kuwa serikali yake itaanzisha maonyesho ya kilimo kwenye kaunti ya Nyamira ili kuwasaidia wakulima kuonyesha mazao yao.
Akihutubu wakati alipozindua rasmi hafla ya kupea matibabu ya bure kwenye shule ya msingi ya Nyamira, Nyagarama alisema kuwa kaunti yake imekuwa ikipoteza mapato mengi kutokana na hali ya watu kushiriki maonyesho ya kilimo kwenye kaunti ya Kisii.
"Serikali yangu ina mipango ya kuinua hadhi ya uwanja wa Nyamaiya ili uwanja huo utumike kwa maonyesho ya kilimo ili kuepusha visa ambapo watu wengi kutoka eneo hili husafiri kwenda Kisii kwa maonyesho ya kilimo, ili nasi tuweze kuinua hadhi ya uchumi wa kaunti hii," alisema Nyagarama.
Nyagarama aliwahimiza wakulima vilevile kuekeza pakubwa kwenye teknolojia ya kisasa kwenye kilimo ili kuhakikisha kuwa wameinua maisha yao kiuchumi kwa kuwa kilimo ni mojawapo ya sekta zinazochangia sana uimarishaji wa mapato nchini.
"Itakuwa vizuri iwapo wakulima wa eneo hili watawekeza pakubwa kwenye teknolojia ya kisasa katika shughuli zao za kilimo kwa maana kupitia hilo wataimarisha maisha yao kwa kuwa kilimo ni mojawapo ya sekta zinazochangia pakubwa ukuaji wa uchumi nchini," alihimiza Nyagarama.
Kwa upande wake mwakilishi wa wadi ya Nyamira mjini Robert Ongwano alisema kuwa iwapo hilo litaafikiwa, basi itakuwa rahisi kwa wakulima wa eneo hili kutangamana na wengine kutoka kaunti za nje na kubadilishana mawazo.
"Hii ni hatua nzuri kwa kuwa wakulima wetu watapata fursa kutangamana na wengine kutoka kaunti zingine na kubadilishana mawazo jinsi watakavyoimarisha maisha yao," alisema Ongwano.