Baada ya kampuni ya ujenzi ya Mock Gardens kutia sahihi mkataba wa shillingi billioni 12 na serikali ya kaunti ya Nyamira ili kujenga jiji la kisasa katika kaunti hiyo, gavana John Nyagarama amesema kuwa hali hiyo itabuni nafasi za kazi kwa vijana.
Akiwahutubia wanahabari nje ya afisi yake wakati wa kuwaaga maafisa wa kampuni hiyo, Nyagarama alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo itabuni nafasi elfu 10 za ajira kwa vijana iwapo mkataba huo wa pamoja utafanikiwa.
"Nina hakika kuwa iwapo mkataba huu wa pamoja utafanikiwa nina hakika kuwa tutaweza kubuni nafasi elfu 10 za ajira kwa vijana wetu kwa maana tutajenga kiwanda cha mabati na hata pia kujenga kituo cha usambazaji stima kwa nguvu za jua," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliongeza kwa kusema kuwa ujenzi wa jiji hilo jipya mjini Nyamira utasaidia pakubwa katika kuwapa makazi wafanyakazi wa serikali ya kaunti hiyo wanaoishi kwenye kaunti zingine.
"Nina hakika kwamba baada ya kumaliza ujenzi wa jiji jipya tunalonuia kulijenga, wafanyakazi wa serikali hii watapata makazi ya kuishi ili waepukane na mzigo wakuishi nje ya mji huu hali ambayo wakati mwingine huwafanya kuchelewa kazini," aliongezea Nyagarama.