Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kuunga mkono marekebisho ya rasimu ya katiba.
Akihutubia waumuni wa kanisa la kiadventista ya Nyamira kusini siku ya Jumamosi, Nyagarama alisema kwamba yafaa rasmu ya katiba ifanyiwe marekebisho ili mgao wa pesa zinazopokezwa serikali za kaunti ziongezwe ili kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Kwa kweli kuna baadhi ya miradi ambayo inahitaji mgao wa pesa za kutosha ili kufadhiliwa, na ndio maana tunataka rasimu ya katiba ifanyiwe marekebisho kwa njia ya kura ya maamuzi ili serikali kuu iongeze pesa za kutosha kwa serikali za kaunti," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliongeza kwa kuwarahi wakristo kote nchini kukumbatia amani na utangamano baina ya jamii mbalimbali taifa hili linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao.
"Kampeni za kisiasa zimeanza mapema tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao na ndio maana nawahimiza wakristo kote nchini kukumbatia amani na utangamano baina ya jamii za kabila mbalimbali," aliongezea Nyagarama.