Kwa mara nyingine tena gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kuwahimiza vijana katika kaunti ya Nyamira kujiunga kwenye makundi ya kujistawisha ili kufaidi kutokana na miradi ya kaunti.
Kwenye mahojiano ya kipekee siku ya Jumatano, Nyagarama alisema kuwa yafaa vijana wajiunge kwenye makundi ya kujistawisha ili kufaidi miradi ya serikali yake.
"Ni ombi langu kwa vijana wa kaunti ya Nyamira kuhakikisha kwamba wanajiunga na makundi ya kujistawisha ili iwe rahisi kwao kunufaika na miradi mbalimbali ya serikali yangu," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliongeza kuwa serikali yake imeafikia mkataba wa pamoja na kampuni ya utengenezaji pikipiki nchini Honda ili kuipa serikali ya kaunti hiyo pikipiki 200 zitakazopokezwa makundi ya vijana ili kujistawisha.
"Asije mtu akasema kwamba serikali yangu imewatenga vijana kwenye miradi ya maendeleo kwa sababu tayari tumeandikisha mkataba na kampuni ya Honda ili itupe pikipiki 200 tukazopokeza makundi ya vijana ili wajistawishe," aliongezea Nyagarama.