Wiki mbili tu baada ya naibu gavana wa kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo kuwarahi wakazi wa kaunti hiyo kuchangamkia upanzi wa miti hasa kwenye msimu wa mvua, gavana Nyagarama vilevile amejitokeza kutilia mkazo suala hilo. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye mkutano wa hamazisho la wananchi kukumbatia kilimo cha unyunyuzi maji mashamba kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumanne, Nyagarama aliwarahi wakazi wa kaunti hiyo kukumbatia upanzi wa miti ili kulinda mazingira. 

"Huu ni msimu wa mvua na ni himizo langu kwa wakazi wa kaunti hii kuhakikisha kwamba wanachukua fursa ya kupanda miti kama njia mojawapo ya kulinda mazingira," alisema Nyagarama. 

Nyagarama aidha aliongeza kwa kuwarahi wazazi kuwaepusha wanao kutokana na kazi za sulubu kwenye muhula huu ambapo shule mbalimbali zimefungwa.

"Wanafunzi wa vyuo na shule nyingi nchini wako manyumbani kwa sababu shule zimefungwa na huenda wazazi wakatumia nafasi hiyo kuwapa wanao kazi za sulubu, ila ni ombi langu kwenu kuhakikisha kwamba hamuwapi watoto wenu kazi nyingi zitakazowanyima saa za kusoma," aliongezea Nyagarama.