Wazazi ambao wamekuwa na mazoea ya kuwakeketa wanao wa kike kwenye kaunti ya Nyamira wameonywa vikali dhidi ya kuendeza hulka hiyo hasa katika msimu huu wa likizo.
Akihutubia waumini wa kanisa la Kiadventista la Nyamaiya kule Nyamira siku ya Jumamosi, Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama alisema mazoea ya kuwakeketa watoto wa kike huwasababishia uchungu mwingi wanapojifungua pindi tu wanapo hitimu utu uzima.
"Watoto wa kike huwa na matatizo makubwa wanapoenda kujifungua kwa kuwa wanapokeketwa inawawia vigumu kujifungua kwa maana wao huhisi uchungu mwingi wanapojifungua," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha amesema kamwe serikali yake haitoruhusu tabia hiyo kushamiri, huku akisema kuwa yeyote atakaye patikana akiendesha tabia hiyo atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
"Chini ya uongozi wangu, hamna mtu hata mmoja atakayeendesha tabia ya kuwakeketa watoto wasichana atakayevumiliwa, na hilo ni onyo kwa yeyote aliye na nia ya kukeketa wasichana hasa kwenye msimu huu wa likizo," alihoji Nyagarama.