Wafanyikazi wa umma kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira ambao hufika kazini kama wamechelewa huenda wakaachishwa kazi mara moja.
Haya ni matamshi yake gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama, aliyetembelea idara mbalimbali za serikali ya kaunti hiyo mapema Jumatano alipozuru maeneo hayo ya kazi ili kutathmini madai ya baadhi ya wafanyikazi kufika kazini wakiwa wamechelewa na kisha kuondoka mapema.
"Wafanyikazi wa umma huajiriwa kuwahudumia wananchi naningependa kuwaonya wale walio na mazoea yakuingia kazini wakiwa wamechelewa na kisha kuondoka mapema kwa hivyo inastahili wajue kuwa tuna wakenya wengine walio na nia yakutoa huduma ambazo wao wanazembea kuzitoa na ninamwagiza msimamizi wa wafanyikazi humu Nyamira kuwachukulia hatua kali watu kama hao," alionya Nyagarama.
Gavana Nyagarama aidha aliwapa changamoto makatibu wa wizara mbalimbali kwenye serikali yake kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inayostahili kutekelezwa na wizara husika inayetelezwa kwa wakati unaofaa.
"Ningependa kuwaomba makatibu wa wizara mbalimbali kuchukua wajibu wakuhakikisha kuwa miradi muhimu ya serikali inatekelezwa kwa wakati unaofaa," alihimiza Nyagarama.