Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewaonya vikali wazazi na walezi wanaoruhusu wanao kutohudhuria shule.
Akihutubia wakazi wa Magwagwa siku ya Jumatatu, Gavana Nyagarama alisema kuwa ni hatia kwa wazazi kuwaruhusu wanao kutohudhuria shule, hali aliyosema itarudisha nyuma taifa hili kimaendeleo.
"Kuna ripoti zinazonifikia kwamba baadhi ya wazazi huwaruhusu wanao kutohudhuria shule, na hiyo ni hatia kubwa kwa maana hali ya watoto kutoenda shule huenda ikaathiri pakubwa ukuaji wa taifa hili," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliwasihi machifu na manaibu wao kushirikiana kuhakikisha kuwa watu wanaoruhusu wanao kutohudhuria shule wanakabiliwa kisheria.
"Kenya ni nchi iliyo na sheria zinazostahili kuzingatiwa, na ndio maana nawasihi machifu na manaibu wao kushirikiana kuhakikisha kwamba wazazi wanaowaruhusu wanao kutohudhuria shule wanachukuliwa hatua za kisheria," aliongezea Nyagarama.
Picha: Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama. Amewaonya vikali wazazi wanaoruhusu wanao kutoenda shule kama inavyostahili. WMaina/Hivisasa.com