Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewarahi wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali za kisiasa kueneza jumbe za amani wanapotafuta kura kwenye kampeni za uchaguzi.
Akihutubu kwenye shule ya upili ya Marindi siku ya Jumapili wakati wa hafla ya kuwapokeza zawadi wanafunzi waliotia fora kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, Nyagarama alisema kuwa yafaa wanasiasa wanaowania nyadhifa za kisiasa wasambaze jumbe za amani wanapotafuta kura.
“Kampeni za kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa zimeanza na ni ombi langu kwa wanasiasa kuhakikisha kwamba wanaeneza jumbe za amani kwenye kampeni zao." alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliongeza kwa kuwarahi wapiga kura kukumbatia amani miongoni mwao, na kutowaruhusu wanasiasa kuwatenganisha kwa kueneza jumbe za chuki.
“Amani inaweza tu kuwepo ikiwa wananchi watakubali kukumbatia utangamano, na ni ombi langu kwao kutowaruhusu wanasiasa kuwatenganisha kwa kusambaza jumbe za chuki miongoni mwao," aliongezea Nyagarama.