Gavana wa kaunti ya Nyamira  John Nyagarama ameshtumu vikali matamshi ya mmoja wa wanachama wa chama cha ODM kuhusiana na uwaniaji wa kiti cha ugavana kupitia tiketi ya chama hicho kwenye mwaka wa 2017. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akimjibu mwanasiasa wa ODM Peter Maroro siku ya Jumanne wakati wa kuwapokea maafisa waliokuwa wakisambaza vyandarua vya kuzuia mbu kwenye maeneo mbalimbali kaunti ya Nyamira jengo kuu la serikali ya kaunti hiyo, Nyagarama alisema kuwa inafaa wanachama wa ODM eneo hilo wamsaidie kutekeleza miradi mbalimbali badala ya kufanya siasa.

"Sio kwamba nakataa kuwa mimi sio mwanachama wa chama cha ODM, lakini ni vizuri kwa wanasiasa kama hao kuunga mkono maswala ya maendeleo badala ya kupiga tu siasa kwa kuwa haistahili viongozi kunitisha na mchujo wa cham cha ODM ikizingatiwa kuwa uchaguzi haujawadia," alisema Nyagarama. 

Gavana Nyagarama aidha alimshtumu Maroro kwa kutaka kuibua vurugu ndani ya chama cha ODM, akisema kuwa nia yake ni kujipa umaarufu wa kisiasa. 

"Sio vizuri kwa Maroro kuendelea kuchochea vurugu ndani ya chama kwa kuwa mimi ni mwanachama niliyejiunga na chama hicho bila kushrutishwa," aliongezea Nyagarama. 

Haya yanajiri baada ya mwakilishi wa wadi ya Manga kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Peter Maroro kujitokeza siku ya Jumatatu na kudhihirisha kutoridhika na uongozi wa gavana Nyagarama.