Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amezihimiza jamii zinazoishi katika mpaka wa Bomet na Nyamira kuishi kwa amani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiwahutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumatano, Nyagarama alisema kuwa yafaa jamii zinazoishi kule Borabu ziishi kwa kutangamana ili kuepukana na visa vya vita baina ya jamii ya Abagusii na ile ya Wakipsigis.

“Amani ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa hili, na ndio maana ningependa kuhimiza jamii zinazoishi katika eneo la mpaka kule Borabu kuishi kwa Amani,” alisema Nyagarama.

Nyagarama aidha aliwaonya vikali watu wanaojihuzisha na visa vya uhalifu katika eneo hilo, huku akihoji kwamba serikali itawachukulia hatua kali za kisheria.

“Kuna watu nasikia kwamba wao ndio wanaovuruga amani ya jamii za Abagusii na Kipsigis wanaoishi katika eneo hilo kwa kujihusisha na uhalifu majira ya usiku, yafaa wajue kwamba siku zao zimehasibiwa na watakabiliwa kwa mujibu wa sharia,” aliongezea Nyagarama.

Haya yanajiri baada ya serikali ya kaunti ya Nyamira kulazimika kufidia mtu wa jamii ya Kipsigis shillingi elfu 100 baada ya watu wasiojulikana kuteketeza tingatinga yake ya kusaga mahindi siku kadhaa zilizopita.