Viongozi wa serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Bomet wameapa kushirikiana ili kumaliza changamoto zinazokumba eneo la Borabu. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakizungumza katika eneo la Chepilat siku ya Jumanne wakati wa hafla yakuchangisha pesa za kusaidia familia zilizofiwa baada ya ajali ya barabarani iliyowauwa watu saba Ijumaa wiki jana, viongozi hao, akiwemo gavana Nyagarama na mwenzake wa Bomet Isaac Ruto, walisema kuwa lazima washirikiane kuhakikisha kuwa kaunti hizo mbili zinaimarika kimaendeleo. 

Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama, serikali yake iko tayari kushirikiana na serikali ya kaunti ya Bomet ili kuhakikisha kwamba usalama na amani miongoni mwa wananchi unaimarishwa. 

"Serikali yangu iko tayari kushirikiana na serikali ya kaunti ya Bomet ili kuhakikisha kuwa usalama na amani unaimarika baina ya wananchi wanaoishi kwenye eneo la Borabu," alihoji Nyagarama. 

Magavana hao wawili walikubaliana kustawisha kaunti hizo mbili kimaendeleo kwa kuwa eneo hilo ni miongoni mwa miji inayotoa kodi nyingi kwa serikali kwa kuwa iko kwenye barabara kuu. 

Eneo la Borabu limekuwa likikumbwa na changamoto nyingi hasa wizi wa mifugo, ukosefu wa usalama na maji safi ya kunywa.