Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewahimiza wananchi kuwajua vyema watu wanaoishi na kutangamana nao ili kuimarisha hali ya usalama kati yao.
Akizungumza na wanahabari baada ya hafla ya kuchangisha pesa za hospitali ndogo ya Borabu siku ya Ijumaa Nyagarama alisema kuwa yafaa wananchi wawajue vyema watu wanaotangamana nao ili kuimarisha usalama miongoni mwao kwa kuwa huenda watu wanaosababisha ukosefu wa usalama wakawa ni wale wananchi wanao wajua vizuri.
"Nawahimiza wananchi kuwajua vizuri watu wanaoishi na kutangamana nao ili kusaidia kuimarisha usalama, kwa kuwa huenda watu walio tishio kwa usalama wakawa wale wanaojulikana vyema na wananchi," alisema Nyagarama.
Gavana huyo aidha aliwahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuwasadia polisi kuwanasa watu wanaotishia usalama wa wananchi, huku akisisitiza kuwa yeyote atakayepatikana akiwasitiri majambazi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
"Nawaomba wananchi washiriakiane na vyombo vya usalama ili kuwasaidia polisi kuwanasa majambazi wanaoendelea kuwahangaisha wananchi, na ninawaonya vikali watu watakaopatikana wakisitiri majambazi kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria," alionya Nyagarama.
Akizungumzia swala la vijana kujiendeleza, Nyagarama aliwahimiza vijana katika kaunti ya Nyamira kujiunga kwenye vikundi na kujisajili kupokea pesa za maendeleo ya vijana almaarufu 'Youth Enterprise Fund', ili kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Kuna pesa za maendeleo ya vijana ambazo serikali inapeana makundi ya vijana ili kujistawisha, na nawahimiza vijana kujisajili kupokea pesa hizo ili kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo," alisema Nyagarama.